Tag Archives: maneno maalumu

Matumizi ya viambishi na maneno maalumu


Viambishi Maalumu

Viambishi maalumu huwa na matumizi ya kipekee katika neno au sentensi. Hapa chini tutachambua aina za viambishi maalumu na mifano yake.


1. Kiambishi ‘ni’

  • a) Nafsi ya kwanza umoja
    Nitafika kesho
  • b) Mahali
    Ameenda nyumabni.
  • c) Kitenzi kishirikishi kipungufu
    Yeye ni daktari.
  • d) Wingi
    Tokeni nje.

2. Kiambishi ‘ndi’

  • Kitenzi kishirikishi kipungufu
    Yeye ndiye aliniibia pesa.

3. Kiambishi ‘ji’

  • a) Udogo
    Kitoto kinalia.
  • b) Ukubwa
    Jibwa limebweka.
  • c) Kirejeshi cha mtenda
    Alijikata makono.
  • d) Nafsi ya pili
    Jinunulie upendacho.
  • e) Kiambishi tamati cha kuundia nomino
    Mwimbaji alituzwa na mgeni wa heshima.

4. Kiambishi ‘Ki’

  • a) Kitendo ki katika hali ya kuendelea
    Tulikuwa tukila alipoingia.
  • b) Masharti/Kitendo kinategemea kingine
    Utapita mtihani ukijitahidi.
  • c) Udogo wa nomino
    Kitoto kinalia.
  • d) Ngeli
    Kiti kimevunjika.
  • e) Kitenzi kishirikishi kipungufu
    Chakula ki mezani.
  • f) Kielezi namna mfanano
    Yeye hutembea kijeshi.
  • g) Kitendo hakifanyiki kamwe
    Kitabu hiki hakisomeki.

5. Kiambishi ‘ku’

  • a) Kikanushi cha wakati uliopita
    Hakunialika.
  • b) Nafsi ya pili umoja
    Alikupigia simu jana.
  • c) Mahali kusikodhihirika
    Huko kungepakwa rangi.
  • d) Ngeli
    Kusoma kwake kunapendeza.

6. Kiambishi ‘ka’

  • a) Mfuatano wa matukio
    Tulikula chakula, tukanywa chai kisha tukalala.
  • b) Vichwa vya habari
    Mwizi kapigwa mawe.
  • c) Kutoa amri
    Kachezeeni nje!
  • d) Kitendo fulani ni tokeo la kingine
    Tulisoma kwa bidii tukapita mtihani.
  • e) Kutoa nasaha/kushauri
    Kamwombe Mola baraka.

7. Kiambishi ‘a’

  • a) Hali isiyodhihirika
    Rais wa Marekaniawasili nchini.
  • b) Vichwa vya habari
    Waziri azomewa na wananchi.
  • c) Kitendo kinaendelea
    Twasoma magazeti.
  • d) Nafsi ya tatu umoja
    Yeye atafaulu sana.
  • e) Ngeli ya A-WA
    Twiga anapendeza sana.
  • f) Kiishio/kauli tenda katika vitenzi
    Anacheza.

8. Kiambishi ‘nge/ngali’ (Masharti Yanayowezekana au Yasiyowezekana)

  • Mfano wa masharti yanayowezekana
    Ningekuwa na pesa, ningenunua kiatu.
  • Mfano wa masharti yasiyowezekana
    Laiti ningalijua nisingaliingia katika hilo basi.

9. Kiambishi ‘po’

  • a) Mahali
    Nionyeshe alipoketi.
  • b) Wakati maalumu
  • Anapotokea wanyama hutoroka.

10. Kiambishi ‘kwa’

  • a) Mahali
    Ameenda kwa Shangazi.
  • b) Jinsi
    Alisoma kwa bidii.
  • c) Sehemu ya kitu
    Amepata alama moja kwa tano katika mtihani.
  • d) Pamoja na
    Mkutano ulijaa wazee kwa vijana.
  • e) Kuonyesha kitu kilitumiwa kama kifaa
    Alikata mkate kwa kisu.
  • f) Sababu
    Aliugua kwa kunywa maji machafu.
  • h) Muda / Kipindi
    Alilia kwa nusu sana.

Maneno Maalumu

Maneno maalumu ni maneno ambayo huwa na matumizi maalumu katika sentensi. Hapa chini, tutachambua maneno maalumu na matumizi yake.


1. Ila

  • a) Isipokuwa
    Watu wote ila yeye wameenda.
  • b) Kasoro
    Hakuna kizuri kisicho na ila.

2. Labda (Pengine / Shaka)

Mfano: Haonekani siku hizi, labda amepata uhamisho.


3. Ikiwa

  • a) (Kama / Shaka)
    Tutamkuta nyumbani ikiwa amepewa likizo.
  • b) Masharti
    Mgonjwa atapona ikiwa atakunywa dawa ipasavyo.

4. Walakini

  • a) Dosari
    Gari limekamatwa kwa sababu lilikuwa na walakini.
  • b) Lakini / Bali
    Amelipa bali hajauziwa.

5. Ingawa / Ingawaje (Hata Kama)

Mfano: Nilienda kazini ingawa sikuwa na nauli.


6. Ijapokuwa / Ijapo / Japo (Hata Kama)

Mfano: Usicheze na nyoka ijapokuwa ni mdogo.


7. Jinsi


a) aina/namna/sampuli
Siwezi kula chakula jinsi hii.
b) kulingana na/kama
Alinilipa jinsi ulivyomwambia


8. Na

  • a) Kiunganishi
    Mama na baba wanalima.
  • b) Umilikaji
    Rhoda ana kitabu kizuri.
  • c) Wakati Uliopo
    Anaandika barua.
  • d) Kauli / Mnyambuliko
    Pate na Simba wanaandikiana barua.
  • e) Kuonyesha Tofauti
    Kiatu hiki ni tofauti na kile.

Hitimisho

Kwa kuelewa matumizi ya viambishi maalumu na maneno maalumu, utaweza kuboresha ufanisi wa matumizi ya lugha ya Kiswahili chako. Endelea kujifunza na kutumia mifano hii ili kuboresha ufanisi wa mawasiliano yako katika Kiswahili!


Share this;