Andika insha MBILI. Insha ya KWANZA ni ya LAZIMA.
Chagua insha moja nyingine kutoka tatu zilizobaki.
Kila Insha isipungue maneno 400.
Kila Insha ina alama 20.
Maswali
- Lazima
Umepewa ratiba ya tamasha za muziki baina ya shule za upili katika eneo lako.Andika shajara ya matukio ya juma moja.
2. Mfumo wa ugatuzi nchini Kenya una faida nyingi kuliko hasara.Jadili.
3. Tunga kisa kitakachodhihirisha maana ya methali ifuatayo:
Mpiga ngumi ukuta ,huumiza mkonowe.
4. Tunga kisa kinachomalizika kwa maneno yafuatayo:
…kwa kweli nilikuwa nimeanguka kitakotako,nilijuta sana!
MWONGOZO WA KUSAHIHISHIA
Umepewa ratiba ya tamasha za muziki baina ya shule za upili katika eneo lako.Andika shajara ya matukio ya juma moja.
- SURA
- Anwani- iwe na maneno: SHAJARA YA TAMASHA ZA MUZIKI KATIKA …
- Anwani iandikwe kwa herufi kubwa.
- Mahali pa kuandalia tamasha hizi patajwe.
- Muda utakaochukuliwa uonyeshwe(juma zima) japo si lazima hapa.
- Siku,tarehe,mwezi na mwaka uandikwe kama vijimada vidogovidogo vya siku zote saba za juma moja.
- Matukio mbalimbali yanayotazamiwa kutekelezwa yaonyeshwe.
- MAUDHUI
Mtahiniwa aonyeshe vitengo mbalimbali vya matukio yatakayoshughulikiwa kila siku.
Mambo haya yahusishwe:
- Kwaya- nyimbo za dini,muziki wa ala/taarab
- Densi za kitamaduni
- Mashairi- Kiingereza,Kiswahili,Kifaransa na lugha nyinginezo. K.m shairi la mtu mmoja,watu wawili.n.k.
Anaweza kutaja aina zozote za ushairi k.v,maghani,malumbano na ngonjera.
- Mazungumzo ya ghafla.
- Kusoma makala
- Michezo ya kuigiza ya kimuziki
*katika vitengo vilivyotajwa mtahiniwa anaweza kugusia maswala ibuka k.v,
- Dawa za kulevya
- Urithi wa wajane
- Ugaidi
- Ukeketaji
- Uchaguzi
- Ufisadi
- Siasa
- Ubaguzi wa kijinsia/ubabedume
- Ajira ya watoto
- Dini
KIELELEZO
SHAJARA YA TAMASHA ZA MUZIKI ZITAKAZOANDALIWA KATIKA SHULE YA UPILI YA LENGA JUU KUANZIA TAREHE 20-27 JUNI 2016.
Jumatatu 20/06/16
Pataandaliwa mashindano ya miziki ya injili,taarab,ala na kitamaduni katika madaraja mbalimbali.Shule kadhaa za wasichana na wavulana zitashiriki.
Jumanne 21/06/16
Densi za kitamaduni katika jamii mbalimbali zitaandaliwa.Densi za Afrika Mashariki zitaandaliwa majira ya asubuhi na za Afrika Magharibi zitaandaliwa mwendo wa alasiri.
Jumatano 22/06/16
Mashairi ya aina mbalimbali yataghanwa na kukaririwa.Mashairi ya Kiingereza yatashughulikiwa majira ya asubuhi,ya Kiswahili na lugha nyinginezo za Kiafrika majira ya alasiri na ya Kifaransa jioni.
Alhamisi 23/06/16
Washiriki watapewa mada fulani fulani za maswala ibuka ili wazijadili chini ya kitengo cha mazungumzo ya ghafla kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Ijumaa 24/06/16
Washiriki watapewa makala fulani kuhusu masuala ibuka ili waweze kuyasoma kwa sauti na ufasaha wa hali ya juu.
Jumamosi 25/06/16
Mashindano ya bendi za kugongana baina ya shule za mseto za eneo hili la Bondeni.
Jumapili 26/06/16
Matangazo ya matokeo.
Kutuzwa kwa makundi yaliyoshinda.
Kufungwa kwa sherehe hii kirasmi.
TANBIHI
- Hiki ni kielelezo tu.Mtahiniwa ana uhuru wa kupanga matukio yake kwa njia nyingine yoyote ile inayokubalika mradi asipotoke.
- Asiandike ratiba.Akifanya hivyo atuzwe bakshishi 01.
- Wajaze angaa pande mbili za karatasi ya majibu.
- Mfumo wa ugatuzi nchini Kenya una faida nyingi kuliko hasara.Jadili.
- Mtahini anastahili kujadili kuhusu faida na hasara za mfumo huu wa uongozi
- Itakuwa bora akitanguliza kwa kueleza maana ya ugatuizi japo si lazima.
- Baada ya kujadili pande zote mbili ,mtahiniwa atoe msimamo wake.
- Mtahiniwa akijadili upande mmoja tu wa swali hili asituzwe zaidi ya alama kumi (10) zilizotengewa swali.
Maana ya ugatuzi
Ni mfumo wa utawala au uongozi ambapo mamlaka huwa yemeenezwa katika majimbo au mashinani ili kuhakikisha kuwa huduma muhimu zimewafikia wananchi kote nchini.
FAIDA
- Unarahishisha uongozi au utawala nchini. Kwa mfano,kila jimbo limekuwa na gavana wake
- Unazalisha nafasi nyingi za ajira hasa mashinani k.m, wawakilishi wa wadi n.k
- Unaimarisha kiwango cha uchumi katika majimbo tofauti kote nchini.
- Unahakikisha kila gatuzi/jimbo linajiendeleza kwa mfano ujenzi wa barabara,hospitali na miundo-msingi mingine.
- Unaboresha kiwango cha elimu katika majimbo yote na nchi kwa jumla.
- Unaimarisha usalama.
- Wananchi wamehusishwa katika utawala.
HASARA
- Mfumo huu unatumia pesa nyingi katika kugharimia mishahara ya wananchi ambao wameajiriwa katika magatuzi mbalimbali.
- Umezua mgogoro kati ya utawala wa kitaifa na utawala wa majimbo.
- Umezua ukabila kwa kuwa Wakenya wanaamini kuwa kila mtu ni sharti aishi na aajiriwe kazi katika jimbo alimozaliwa na kulelewa.
- Majimbo mengine yamekosa kuendelea kutokana na uongozi mbaya.
- Majimbo mengine yamebakia nyuma kimaendeleo kwa sababu hayana rasilimali za kutosha.
- Ufisadi umekithiri.
- Ubadhirifu wa pesa za umma k.m,starehe nyingi k.v,ziara katika mataifa ya nje zisizo na faida yoyote.
- Ahadi zisizotimizika.
- Tunga kisa kitakachodhihirisha maana ya methali ifuatayo:
Mpiga ngumi ukuta ,huumiza mkonowe.
- Mada iwe methali hii.Akiandika anwani tofauti aondolewe alama za mtindo.
- Si lazima atangulize kwa kueleza maana ya methali hii.Si kosa akifanya hivyo.
- Ashughulikie pande zote mbili za methali.Asipofanya hivyo ,asituzwe zaidi ya alama 10.
- Asimulie kisa kinacholenga maana ya methali hii.
Maana: Ajitakiaye msiba hana kilio labda alie na mizimu wake tu.
Matumizi: – Hutumiwa kumnasihi na kumwonya mtu asishindane na mtu anayemzidi uwezo kwa kuwa akifanya hivyo atajiumiza bure.
- Anayejitakia msiba kisha akaanza kuwalaumu wengine kwa kutomsikitikia ndiye huambiwa methali hii.
- Tunga kisa kinachomalizika kwa maneno yafuatayo:
…kwa kweli nilikuwa nimeanguka kitakotako,nilijuta sana!
- Aandike kichwa – abuni na kisizidi maneno sita.
- Asiongeze au adondoe neno au herufi katika mdokezo huu.Akifanya hivyo atuzwe bakshishi 01.
- Lazima maneno ya mdokezo yaje mwisho kabisa.
- Mtahiniwa asimulie kisa kitakachohusisha mhusika ambaye mambo yamemharibikia au kumwendea kombo kwa sababu ya kosa lake mwenyewe.
Au
- Asimulie kisa kuhusu mhusika ambaye alikuwa amenawiri kimaisha baadaye mafanikio yake kusambaratika kwa sababu ya mwelekeo potovu aliouchukuwa.
UKADIRIAJI NA UTUZAJI
Alama
Maneno 174 Insha robo ____________04-05
Maneno 175-274 Insha nusu ____________ 10
Maneno 275-374 Insha robo tatu ____________15
Maneno 375 na kuendelea Insha kamili ____________ 20
Maudhui | 07-08 A | 05-06 B | 03-04 C | 01-02 D |
Jumla ya Upeo | 16-20 | 11-15 | 06-10 | 01-05 |